|
Friday, 14 May 2010 11:24 |
|
*Yafungiwa ndani ya kibanda porini *Mtekaji anyonga kichanga *Adaiwa kutumia silaha, mbwa, manati na panga
Na Benedict Kaguo, Tanga WATU wanne wa familia moja wametekwa nyara na mkazi mmoja wa Kijiji cha Kijerwa Hemsambia Kata ya Kigongoi wilayani Mkinga Mkoani Tanga na kisha kufanikiwa kumnyonga mtoto wa mdogo mwenye umri wa miaka minne ambaye ni mpwa wake. Mtekaji nyara huyo, Mwajego Jumaa, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20, aliifungia familia hiyo ndani ya kibanda porini kwa muda wa siku tatu mfululizo kisha kumuua mtoto mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.
Baada ya kutekeleza mauaji hayo, kijana huyo aliichukua maiti ya mtoto huyo na kuiingiza kwenye mfuko wa kiroba na kisha kuitupa porini. Kijana huyo anasadikiwa kutumia silaha mbalimbali likiwamo panga, upinde, manati na mbwa wanane katika kufanikisha kazi hiyo ya utekaji nyara huo, akiwamo dada yake, kaka na wapwa zake wawili. Kufuatia tukio hilo, wananchi wa Kijiji hicho walitoa taarifa katika kituo Kikuu cha Polisi Maramba ambapo Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) walikwenda kijijini hapo na kisha kufanikiwa kumtia mbaroni. Mmoja wa wananchi wa Kijiji hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini alidai kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa tatizo la ugonjwa wa akili na inadaiwa alikuwa akijihusisha na kilimo cha zao la bangi katika shamba lake. Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga, Jaffar Mohamed, Amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa kwa sasa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na Polisi huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea. Mohamed alisema mara baada ya uchunguzi huo kukamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
|