FAHAMU HAKI NA WAJIBU WAKO KWA MUJIBU WA SHERIA ZA ARDHINa Wakili Justine Kalebo
Watu wengi wameonewa, kudhulumiwa na kunyanyaswa katika ardhi zao wenyewe kwa sababu ya kutojua haki na wajibu wao. Hakuna kitu kibaya sana na cha kushangaza kama mwenyeji ukaonewa na kunyanyaswa na mgeni katika ardhi yako mwenyewe kwa sababu tu hujui haki zako ni zipi kisheria. 


Sheria za ardhi zinaeleza juu ya haki ulizo nazo. Ni wajibu wako kuzifahamu ili uweze kujua namna ya kuzipata. Haki na wajibu wako kwa mujibu wa sheria zinaanzia katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho, ambayo inakupa haki yako ya kimsingi ya kumiliki mali ambazo ni pamoja na ardhi (ibara ya 24). 


Sheria za ardhi zinaeleza wazi kuwa haki zako ni pamoja na; Kupatiwa umiliki au urithi  wa ardhi bila kujali jinsia yako uwe mwanamke au mwanaume. Mwanamke kuwa na mamlaka ya kutumia, kuuza au kutoa ardhi kama ilivyo kwa mwanamume. Kupatiwa hati ya umiliki wa ardhi yenye jina, sahihi na picha yako mara baada ya kumilikishwa ardhi. 


Kuuza, kununua, kutoa au kubadilisha umiliki baada ya kujiridhisha juu ya umiliki halali wa yule anaye kuuzia. Kukata rufaa kutoka katika chombo kimoja cha sheria hadi kingine endapo utakuwa hujaridhika na maamuzi yaliyotolewa na chombo husika. 


Kuweka rehani au dhamana ardhi yako kwa ajili ya kujipatia kipato au shughuli za kibiashara. Kutoingiliwa katika eneo lako unalolimiliki kisheria. Kulipwa fidia stahiki inayoendana na thamani ya ardhi pamoja na mazao au jengo lililopo katika ardhi hiyo endapo eneo lako litachukuliwa na serikali kwa ajili wa matumizi ya umma au shughuli nyingine yoyote. 


Kumiliki ardhi kwa pamoja au kibinafsi kati ya mke na mume. Kupata nakala za mikataba ya au hati yoyote ya umiliki wa yule anayekuuzia, anayekupa au anayekukabidhi ardhi hiyo mara baada ya makabidhiano au mauzo ya eneo hilo.


Sheria za ardhi pia zimeainisha wajibu wako ambao ni muhimu sana ukaufahamu ili uweze kuutimiza na kukupa uwezo wa kudai haki zako. Wajibu wako ni pamoja na; Kuliendeleza na kulitunza eneo ulilopatiwa kisheria. Kufanya matumizi sahihi na halali yaliyoidhinishwa katika masharti maalum ya utoaji wa ardhi hiyo na kutobadilisha matumizi ya eneo ulilopatiwa pasipo idhini ya mamlaka husika. 


Kufungua shauri la ardhi katika vyombo vya sheria ndani ya muda usiozidi miaka 12 baada ya  mgogoro kutokea, ikizidi hapo utakuwa umepoteza haki yako. Kutambua mahali kiwanja chako kilipo na chombo gani kina mamlaka ya kutatua migogoro ya ardhi katika eneo hilo. Kujiridhisha juu ya haki na mamlaka ya umiliki wa yule anayekuuzia ardhi hiyo katika ofisi za ardhi au uongozi wa serikali uliopo katika mtaa, kata, kijiji au wilaya husika. 

Kulipa kodi za ardhi na majengo yaliyopo katika ardhi hiyo. 


Kutofanya au kutoruhusu kufanyika vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria katika eneo unalolimiliki. Kutouza eneo ulilopatiwa kisheria pasipo kuitaarifu mamlaka husika iliyokumilikisha. Kutoa taarifa katika mamlaka husika pale unapoona kuna matumizi mabaya ya ardhi yanafanyika. 


Fahamu haki zako, timiza wajibu wako. Usikubali kuonewa au kudhulumiwa wakati sheria imetungwa kulinda haki zako. Chukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.


KWA MAELEZO ZAIDI JIPATIE KITABU CHA JUKWAA LA SHERIA AU THE PLATFORM OF LAW. FIKA OFISINI KWETU - POSTA MPYA JENGO LA MAVUNO HOUSE - GHOROFA YA 1, OFISI NAMBA 102 AU TUPIGIE SIMU NO. 0756636264 / 0714636264. KARIBU

No comments

Powered by Blogger.