HII HAPA NAMNA BORA YA KUWEKEZA KWENYE HISA ZA MAKAMPUNINa Wakili Justine Kalebo 

Kuwekeza ni jambo zuri sana hasa ikiwa uwekezaji wako umeufanyia utafiti wa kutosha na kujiridhisha kuwa utakulipa bila kujali hatari zinazoweza kujitokeza katikati. Unapoamua kuwekeza maana yake umeamua kuinunua kesho yako. Umeamua kuiwekea kinga kesho yako na umeamua kupanda mbegu ya muda mrefu itakayoota na kuzaa matunda yatakayodumu muda mrefu.


Uwekezaji huhitaji fikra za kijasiriamali. Fikra za kitajiri. Fikra zenye uwezo wa kuona mbali kama tai na kuchukua hatua kukiendea kile ulichokiona. Kuwekeza hakuhitaji pupa, papara, haraka wala kuiga. Kunahitaji hesabu, utulivu, utafiti na kujitoa mhanga. Unapoamua kuwekeza unahitaji kutulia na kufanya tathmini ya kina iili karata yako iende mahakli sahihi patakapoleta manufaa. Maamuzi yako hayapaswi kuwa ya kufuata mkumbo wala yasiyo na taarifa za kutosha bali maamuzi yako yanapaswa kuwa ni matokeo ya taarifa zilizochakatwa na kuchujwa na hatimaye kupata taarifa zenye uwezo wa kukufanya ufanye maamuzi yatakayobeba hatima za kizazi cha sasa na kizazi kijacho.


Kwa mujibu wa sheria, uwekezaji kwenye hisa ni haki ya kila mmoja. Iwe ni mtu binafsi, kampuni au taasisi yoyote ile inaruhusiwa na inayo haki ya kuwekeza kwenye hisa. Hisa si kwa ajili ya watu fulani pekee, hapana. Ni kwa ajili ya watu wote wanaotaka kuzituma pesa zao zifanye kazi badala yao na sio wao kuwa watumwa wa kufanya kazi kwa ajili ya pesa. Achana na fikra potofu kwamba hisa ni kwa ajili ya matajiri, wasomi au wafanyakazi au watu wa kada Fulani tu, hapana uwekezaji kwenye hisa ni haki ya kila mmoja na kila mtu au taasisi ikiwemo taasisi za kijamii au za kidini pia zinaweza kuitumia vizuri fursa ya kuwekeza kwenye hisa na hatimaye kuleta manufaa.


Japokuwa uwekezaji wa hisa kupitia taasisi unapaswa kuwa ni uamuzi wa kitaasisi na si uamuzi wa mtu mmoja au mtu binafsi ni muhimu sana uongozi wa taasisi ukawa na taarifa za kutosha ikiwa ni pamoja na kuwaeleimisha wadau wote katika taasisi ikiwezekana hata kwa kutoa elimu kwa kila mdau ili wanapofanya maamuzi wawe wana taarifa za kutosha na wafanye maamuzi sahihi.


Kwa mujibu wa sheria ya Makampuni Sura ya 212 ya mwaka 2002 pamoja na sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana sura namba 79 ya mwaka 2002; Hisa ni sehemu ya rasilimali za kampuni. Hisa ni umiliki wa kampuni. Kununua hisa ni kununua sehemu ya umiliki wa kampuni husika. Huwakilisha maslahi yako kwenye kampuni husika.


Ili upate pesa huhitaji kuwa mwendeshaji wa kampuni unahitaji tu kuwa mmiliki wa kampuni kwa kununua hisa zake. Hisa ni mtaji. Hisa ni rasilimali au kitega uchumi. Hisa ni mali fedha. Hisa ni biashara, unaweza kufanya biashara ya hisa kwa kuuza na kununua.


Hisa ni dhamana, hukupa uwezo wa kukopa kwenye taasisi za fedha kwa kutumia cheti cha umiliki wa hisa. Hisa ni akiba, unaponunua hisa unaweka akiba ya fedha zako.


Kuwekeza kwenye hisa ni rahisi sana. Huhitaji kuwa na fedha nyingi bali unahitaji kufanya utafiti mwingi na kuwa na fikra za kitajiri sio za kimaskini. Hata ukiwa na kiasi kidogo sana cha fedha unaweza ukaanza kununua hisa. Huhitaji mamilioni, unahitaji maarifa ya namna ya kuwekeza.


Hisa huuzwa na makampuni ambayo yamesajiliwa na kuorodheshwa na soko la hisa la Dar es salaam. Kuna kampuni zaidi ya kumi mpaka sasa ambazo zinauza hisa zake. Hizi ni pamoja na TBL, TCC, CRDB, NMB, TWIGA, SWISSPORT, KCB, DCB, TTB, TWIGA, TOL, TTP, SIMBA na nyinginezo. Hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya kisheria ambayo yamezitaka kampuni za uwekezaji kwenye madini na mawasiliano kuhakikisha kuwa zinaingia kwenye orodha ya kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es salaam. Ndio maana hivi karibuni kampuni ya VODACOM imeonyesha mfano na nyingine zitafuata katka mlolongo huo.


Ukiacha kwamba thamani ya hisa zako huweza kupanda, lakini pia kampuni hizi zinaweza kutoa gawio kila mwaka kutegemeana na kiwango cha faida kilichopatikana na idadi ya hisa unazomiliki.


Hisa huuzwa na mawakala waliosajiliwa na kuidhinishwa na soko la hisa la Dar es salaam ambao hupokea fedha zako na kukupatia idadi ya hisa unazohitaji kulingana na fedha ulizotoa. Pia wao huhusika kukuuzia hisa zako endapo utahitaji kuuza hisa zako.


Mawakala hawa husaidia kupatikana kwa cheti cha umiliki wa hisa zako baada ya kununua. Pamoja na gharama utakayowalipa lakini ni ndogo sana ambayo huwa haizidi asilimia 2.5 ya thamani utakayonunua.


Mchakato wa kuuza hisa zako pia umerahisishwa kwa kutumia mawakala hao hao ambapo utapaswa kuwasilisha ombi lako kwa mawakala hao ili wao waweze kuona mteja yupi anahitaji kununua hisa hizo na katika utaratibu gani ili uweze kufanyika kwa manufaa. Ni muhimu kuuza wakati thamani imeongezeka ili hisa zako zilete faida.


Ukombozi wa maisha yako uko mikononi mwako. Kesho yako inaandaliwa leo. Maisha bora hayaletwi na wanasiasa, yanaletwa na wewe binafsi. Chukua hatua za ukombozi wako kiuchumi. Safari ya maili 1000 huanza na hatua moja. Chukua hatua na uanze kuwekeza kwenye hisa. Kila mtanzania anayo haki kisheria ya kuwekeza.

JUSTINE KALEB - 0755545600 / 0713636264)

ADVOCATE JUSTINE KALEB

CEO/LEGAL CONSULTANT

MORIAH LAW CHAMBERS,

MAVUNO HOUSE - POSTA MPYA,

(OPPOSITE TO TOTAL PETROL STATION),

1ST FLOOR - OFFICE NO. 102,

P.O. BOX 70849,

DAR ES SALAAM - TANZANIA - EAST AFRICA.

MOB: +255 755 545 545 600 / +255 713 636 264

TEL: +255 222 110 684

EMAIL: moriahclients@gmail.com

FACEBOOK: Moriah Law Chambers

No comments

Powered by Blogger.