FAHAMU NAMNA BORA YA KUVUNJA MKATABA WA KAZI

Picha na MtandaoniNa Wakili Justine Kalebo

Mkataba wa ajira husainiwa kwa amani, nderemo, vifijo na shukrani nyingi huku nyuso za pande zote mbili yaani mwajiri na mfanyakazi zikionyesha furaha ya kufungua ukurasa mpya wa maisha kwa kutenda kazi pamoja. Mwajiri huwa na matarajio makubwa na mfanyakazi naye huwa na matarajio makubwa ya maisha bora, kutimia kwa malengo yake na malipo stahiki.


Tatizo hutokea pale upande mmoja unapoanza kuonyesha dalili za kutaka kuvunja mkataba wa kazi. Hata kama mkataba una vipengele vya namna ya kuvunjwa kwake lakini mara nyingi hizo huwa ni habari mbaya kwa pande zote mbili. Usipokuwa makini unaweza ukavunja mkataba kiholela na kukugharimu fedha nyingi na usumbufu mkubwa ambao unaweza kuepukika ukifuata sheria.


Sheria za mikataba sura namba 345 ya mwaka 2002, sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 na kanuni zake; zinaeleza kuwa, mkataba wa kazi unaweza kuvunjika kwa wahusika kufariki, matakwa ya kisheria, mfanyakazi kujiuzuru, makubaliano ya amani ya kuvunja mkataba kati ya mwajiri na mfanyakazi, mfanyakazi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai au mfanyakazi kushindwa kufanya kazi kwa sababu za kiafya. Mwajiri anaweza kumfukuza au kumwachisha kazi mfanyakazi kutokana na utovu wa nidhamu, mfanyakazi kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi au sababu za uendeshaji wa taasisi. 


Sheria inamruhusu mfanyakazi kuvunja mkataba wa ajira. Mfanyakazi atapaswa kufuata matakwa ya vipengele vilivyoko katika mkataba wake wa kazi ili aweze kuvunja mkataba wake wa kazi na mwajiri. Sheria imeweka wazi taratibu hizo kuwa ni pamoja na mfanyakazi kutoa taarifa ya maandishi ya mwezi mmoja kabla au mfanyakazi kumlipa mwajiri mshahara wake wa mwezi mmoja endapo atatoa taarifa ya masaa 24 ya kuvunja mkataba. Ukiacha malipo ya kiinua mgongo mfanyakazi aliyevunja mkataba bado ana haki ya kulipwa haki zake zote kama wafanyakazi wengine kwa mujibu wa sheria.


Kwa upande mwingine, mwajiri naye ana haki ya kuvunja mkataba. Lakini ni muhimu sana mwajiri akatafakari kwa kina maamuzi yake ya kuvunja mkataba na kuhakikisha kuwa sababu zake ni msingi, halali na zimezingatia kanuni za haki sawa na zinakubalika kisheria, vinginevyo inaweza kumgharimu pesa nyingi na usumbufu mkubwa ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya sheria. Usivunje mkataba wa kazi kwa jazba, kwa kumkomoa mfanyakazi, kwa maslahi yako binafsi au kwa sababu isiyokubalika kisheria. Itakugharimu sana. Ni muhimu kuomba ushauri kwa wataalamu wa sheria ili waweze kukujulisha namna bora unayoweza kuvunja mkataba wa kazi pasipo kusababisha madhara wala hasara ya namna yoyote ile kwa pande zote mbili. 


Kumbuka mfanyakazi aliyeachishwa kazi isivyo halali ana haki ya kulipwa mishahara yake yote ya muda ambao hakuwepo kazini, mshahara wa mwezi mmoja badala ya notisi, malimbikizo ya likizo, kiinua mgongo, malipo ya usafiri, mafao ya hifadhi ya jamii, cheti cha utumishi, fidia ya mishahara ya miezi 12 na malipo mengineyo. 


Ukitumia nguvu, sheria itakuzidi nguvu. Kama mtu ameweza kufanya kazi na wewe kwa muda wote huo, kwa nini usithamini utu wake na mustakabali wa maisha yake na familia yake. Vunja mkataba wa kazi kisheria, kistaarabu na kiungwana, ili kesho ukihitaji tena kufanya kazi na mtu huyo usipate ugumu wa kumpata au kupata kazi.


Kwa Ushauri zaidi unaweza kufika katika ofisi zetu zilizopo, Dar es salaam, Posta Mpya, Jengo la Mavuno House, Ghorofa ya 1, Ofisi Na. 102B. Kwa mawasiliano zaidi au msaada wa kisheria, wasiliana nasi kwa anwani ifuatayo:-

Mkurugenzi Mkuu,

Moriah International Foundation,

Idara ya Msaada wa Kisheria,

P.O. Box 70849,

Dar es salaam.

Simu: +255 713 63 62 64 / +255 755 54 56 00 / +255 222 110 684

Email: jukwaalasheria@gmail.com / moriahlawyer@gmail.com

Facebook: Jukwaa La Sheria

No comments

Powered by Blogger.